Wadau wa sekta ya utalii nchini wamepongeza hatua ya kuzindua upya maeneo ya kuegesha meli za kitali katika Bandari ya Mombasa.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa, mwenyekiti wa kitaifa wa muungano wa watalii Pwani Mohammed Hersi alisema uzinduzi huo utachangia katika kuimarisha zaidi sekta ya utalii pamoja na uchumi wa nchi kwa jumla.
Hersi alisema kuwa hatua hiyo ni muhimi sana kwa kuwa mara nyingi meli za watalii zilikuwa zikikosa mahali pa kuegeshwa.
Aliipongeza serikali kwa uzinduzi huo na kuongeza kuwa wanatarajia idadi kubwa ya watalii kuwasili katika bandari ya Mombasa hususan mwezi huu wa Disemba.
“Sekta ya utalii ni sekta muhimu iliyotegemewa kiuchumi humu nchini na hivyo ipo haja ya serikali kuwekeza na kuiboresha sekta hii zaidi,” alisema Hersi.