Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Mombasa Bi Mishi Mboko ameitaka serikali ya Jubilee kuheshimu upande wa upinzani katika utendakazi wake.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa, Mboko alisema kuwa upande wa upinzani una haki kidemokrasia kupinga na kukosoa utendakazi wa serikali pindi inapokosea bila kuhujumiwa.
Mboko alisema kuwa ni jambo la kustaajabisha kuona jinsi serikali inavyolaumu upande wa upinzani kwa kuwakosoa, hatua aliyoitaja kudhihirisha kuwa Jubilee imeshindwa kuwajibikia majukumu yake kikamilifu.
Mwakilishi huyo aidha alisema kwamba kuna haja ya pande hizo mbili kushirikiana vyema kwenye maswala ya uongozi, ili kuhakikisha kwamba taifa linapiga hatua mbele na wananchi wananufaika kimaendeleo.
Wakati huo huo, amewataka wakaazi wa ukanda wa Pwani kuwa macho zaidi wakati huu wa uchaguzi mkuu na kujitenga na viongozi wanafiki wenye sera za kuwachanganya.