Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakaazi wanaotumia kivuko cha Likoni wanaendelea kutoa hisia kinzani kutokana na hatua ya kusimamishwa kazi kwa mkurugenzi mkuu wa shirika hilo Musa Hassan.

Baadhi ya wakaazi hao waliunga mkono hatua hiyo huku wengine wakionekana kutoridhishwa.

Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Alhamisi katika kivuko hicho, baadhi ya wakaazi hao wanasema kuwa kuna mambo mengi ambayo yangefaa kushughulukiwa na wala sio kumsimamisha kazi mkurugenzi huyo.

“Mimi sioni kama kumfuta kazi itasaidia. Suluhisho hapa ni kurekebisha feri ama sivyo kununuliwe zingine mpya kwa sababu bila hatua hiyo, hata wakileta mkurugenzi mwingine bado shida ni ile ile tu,” alisema mmoja wa wakaazi aliyejitambulisha kama Omar.

Wengine nao wanaamini kuwa matataizo ya feri ni kutokana na uongozi mbaya na hivyo kuunga mkono kusimamishwa kazi kwa mkurungezi huyo.

“Hapo wamefanya jambo zuri sana. Hatua ya kwanza ni hiyo ya kumsimamisha mkurugenzi kazi kwa sababu yeye ndio kizingiti kikubwa hapa,” alisema Bi Agness Wakio, mkaazi.

Mkurugenzi wa Kenya Ferry alisimamishwa kazi kwa muda siku ya Jumatano baada ya kikao maalum kilichofanywa na washikadau siku chache baada ya Rais Uhuru Kenyatta kuzuru eneo hilo mapema wiki hii, huku zoezi la kutafuta suluhu likiendelea.