Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC imeelezea hofu kuwa huenda ikasajili idadi ndogo ya wapiga kura katika eneo la Pwani kufuatia madai kuwa vuguvugu la MRC linawashawishi wakaazi kususia usajili huo.
Akiongea na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Kamishina wa IEBC kanda ya Pwani kazkazini Amina Sudi alisema kuwa tangu zoezi hilo lianze, idadi ndogo ya wakaazi imeonekana kujitokeza na kujisajili katika zoezi hilo, na kusema kuwa huenda tume hiyo ikose kufikia malengo yake.
Sudi alisema kuwa maafisa wa IEBC wanaofanya usajili huo mashinani wamekuwa wakikumbwa na changamoto kwani baadhi yao wamekuwa wakifurushwa na baadhi ya wakaazi ambao wanashukiwa kuwa wanachama wa MRC.
Aidha, alitaja maeneo ya Kaloleni na Rabai kama maeneo yanayokumbwa na changamoto hizo.
Alisema ukosefu wa hamasa kwa wananchi wanaoishi mashinani kumechangia hali hiyo na usajili huo huenda ukakumbwa na utata zaidi.
"Tuko na hofu kuwa zoezi hili kuenda likakatizwa kutokana na vitisho kuwa huenda vuguvugu la Mombasa Republican Council (MRC), likavuruga usajili huo kwani tayari baadhi ya maafisa wetu wamefurushwa katika vituo vya usajili wa wapiga kura na wafuasi wa kundi hilo,” alisema Sudi.
Kamishna huyo amezidi kuwashinikiza wananchi wa eneo nzima la Pwani kujitokeza katika usajili huo kwani ndio mwanzo wa kuleta mabadiliko katika taifa hili.