Wanafunzi wengi katika vyuo vikuu wameonyesha hofu kutokana na shambulizi lililotekelezwa na wanamgambo wa Al Shabaab katika chuo kikuu cha Garissa siku tatu zilizopita. Wanafunzi, kupitia mitandao ya kijamii, wameeleza kutoridhika kwao na jinsi usalama unavyokabiliwa nchini. Felix Sammy Syommane ni mmoja kati ya viongozi wa wanafunzi wa chuo kikuu cha Maseno. Katika ujumbe alioutuma katika mtandao wa kijamii wa Facebook, Sammy alisema kwamba ni jambo la kuhuzunisha kwa wanafunzi ambao wamejikaza na masomo na kufika katika vyuo vikuu kuuawa kinyama. “Wengi wetu wanatoka katika familia hohe hahe na wanasaidiwa na jamii zao ili kupata hata karo,” alisema. Huku wengi wakishikilia kwamba serikali iondoe majeshi ya Kenya kutoka Somalia, Francis Okwara, naibu mwenyekiti wa muungano wa wanafunzi katika chuo kikuu cha Maseno (SOMU) amesema kwamba si jambo la busara kufanya hivyo. “Jeshi la Kenya likitolewa Somalia, itamanisha kwamba Kenya imeshindwa na vita dhidi ya ugaidi na hili litawapa motisha magaidi,” alisema Okwara. Hali ya hofu bado imetanda katika vyuo vingi vikuu huku picha zikisambaa kwamba huenda Chuo Kikuu cha Egerton kikavamiwa hivi karibuni. Willy Moroga ameeleza hisia zake kupitia ujumbe aliotuma katika ukurasa wa 'CPP CAMPUS POLITICS PLATFORM - MASENO UNIVERSITY'. Kulingana na Moroga, hakuna mwanafunzi aliye salama. Amekitaka chuo kikuu cha Maseno na viongozi wake kuweka hatua madhubuti ili kukabiliana na visa ambavyo huenda vikasababisha ukosefu wa usalama. Hata hivyo, wengi wao wamewasihi wakenya kusimama imara na kutupilia mbali tofauti zao za kisiasa na kidini ili kukabiliana na ugaidi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know