Hospitali nyingi za ukanda wa Pwani zimeripotiwa kukumbwa na uhaba wa damu kufuatia kuongezeka kwa ajali za barabarani hasa wakati huu wa likizo.
Kwenye mahojiano na mwandishi huyu kwenye kituo cha kutoa damu mjini Mombasa siku ya Jumatano, Kenneth Otieno, ambaye ni mmoja wa afisa katika kituo cha kuhifadhia damu cha ‘Coast Regional Blood Transfusion Centre’ alieleza hofu yake kuwa huenda hali hiyo ikawa mbaya zaidi iwapo wakazi hawatajitokeza kutoa damu.
“Hospitali za ukanda wa Pwani kwa sasa zinapitia changamoto ya uhaba wa damu. Kwa kawaida wanafunzi ndio huchangisha damu kwa wingi, lakini kwa sasa shule zimefungwa hivyo hali imekuwa mbaya sana,” alisema afisa huyo.
Kulingana na afisa huyo, idadi kubwa ya wagonjwa wanaohitaji damu ni wale wanaofanyiwa operesheni na wanawake wanaojifungua.
Aidha, Otieno aliwahimiza wakaazi mjini humo kujitokeza kutoa damu ili kusaidia kukabiliana na hali hiyo.