Baada ya lalama kutoka kwa wakaazi wanaoishi pambizoni mwa hospitali ya kijamii ya Bomu huko Magongo katika eneo la Changamwe, sasa mbunge wa eneo hilo Omar Mwinyi ameingilia katika mgogoro huo.
Mwinyi amesema kuwa amechukua hatua hiyo ili kutafuta mwafaka kati ya wakaazi na usimamizi wa hospitali hiyo ya kijamii ambapo huenda mgogoro huo ukapamba moto iwapo hautatatuliwa.
Mwinyi amelalamikia hali ya uchomaji taka zinazotokana na shughuli za hospitali hiyo bila ya mpangilio mwafaka wala kuzingatia hali ya mazingira.
Aidha, ameihimiza hospitali hiyo kushukisha gharama za kimatibabu kwa wakaazi wanaotafuta huduma za kimatibabu katika hospitali hiyo hasa baada ya akina Mama wanaojifungua katika hospitali hiyo kulalamikia kutozwa kiwango cha juu cha pesa.
“Tumeamua kuingilia kati swala hilo ili kuhakikisha kuwa wakaazi wa eneo la Changamwe wanapata huduma bora za kiafya katika hospitali hiyo ya Bomu kwa ushirikiano mwema na wasimamizi wa hospitali ya Bomu,” alisema Mwinyi siku ya Jumamosi baada ya kukutana na wakaazi na wasimamizi wa hospitali hiyo.
Kwa upande wake, mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo Daktari Hamid Abeid amewahakikishia wakazi hao kuwa maslahi yao yote yatazingatiwa na usimamizi wa hospitali hiyo.