Hospitali ya Mama Lucy imeondolewa lawama na jopo lililoteuliwa kuchunguza kifo cha mtoto wa miezi mitatu kilichotokea katika hali ya kutatanisha kwenye hospitali hiyo.
Mwenyekiti wa jopokazi la watu tisa lililobuniwa kuchunguza madai ya utepetevu wa wafanyikazi wa hospitali hiyo, Philip Kungu alisema kuwa mwendazake alipokea huduma zilizohitajika katika hospitali hiyo.
Kungu alikiri kuwepo kwa ukosefu wa ambulensi iliyofaa kumsafirisha mtoto huyo hadi hospitali kuu ya Kenyatta kupokea matibabu zaidi.
‘'Tulizungumza na watu wote wanaohusishwa na kisa hiki, wakiwemo wauguzi katika hospitali hiyo uongozi wa hospitali hiyo na pia familia ya mwendazake na tumebaini kwamba marehemu, Dominic alipewa matibabu yaliyohitajika na yaliyokuwepo kwa wakati huo,'’ alisema Kungu.
Kungu, ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi ya huduma za umma katika kaunti ya Nairobi, aliweka wazi kuwa mtoto huyo aliyeaga alikuwa amesafirishwa kutoka kwa kituo kingine cha afya akiwa katika hali mahututi ambapo madaktari katika hospitali hiyo ya Mama Lucy walimuhudumia ila vyombo vya habari vilitilia mkazo masaa yaliyochukuliwa kusubiri ambulensi ya kumkimbiza mtoto huyo katika hospitali kuu ya Kenyatta kitengo cha waonjwa mahututi almaarufu ICU.
Jopokazi hilo sasa linapendekeza kujengwa kwa kitengo cha kutoa matibabu kwa wagonjwa mahututi cha ICU na HDU hospitalini humo ili kuzuia visa kama hivyo kutokea tena na kurekebishwa kwa magari mawili ya ambulensi ya hospitali hiyo ambayo hayafanyi kazi kwa sasa.
Mtoto huyo aliaga dunia tarehe 10, Februari, 2016 akisubiri kusafirishwa hadi hospitali kuu ya Kenyatta jijini Nairobi kupokea matibabu zaidi katika kile kilichodaiwa kuwa utepetevu wa wafanyikazi wa hospitali hiyo.