Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Nakuru imetoa dawa zenye thamani ya Sh52m kwenye hospitali na vituo vya kimatibabu vinavyopatikana kwenye kaunti hiyo.

Dawa hizo zilizonunuliwa kutoka kwa mamlaka ya dawa ya Kemsa na serikali ya Kaunti ya Nakuru zinalenga kufikishwa kwenye hospitali na vituo hivyo vya kimatatibabu siku ya Jumatano.

Akizungumza siku ya Jumatatu kwenye makao makuu ya Kaunti ya Nakuru, Gavana Kinuthia Mbugua alisema kuwa kaunti ya Nakuru haijawahi kukumbana na uhaba wa dawa.

Mbugua alisema kuwa dawa hizo zitapelekwa katika hospitali nane kuu zilizoko katika kaunti hiyo.

“Serikali ya Kaunti ya Nakuru imepiga hatua kubwa katika maisha ya wakazi. Hatua hii inaashiria kujitolea kwetu. Vituo vya kimatibabu vya kaunti havitawahi kukosa vifaa vya kimatibabu,” alisema Mbugua.

Aidha, Gavana Mbugua alisema kuwa kaunti ya Nakuru imebahatika kupata hospitali nane ilhali baadhi ya kaunti hazina hospitali.

“Kaunti hii yetu ina bahati kwa sababu tuna hospital nane. Kuna kaunti ambazo hazina hospitali hata moja. Dawa hizi zitaweza kutumika kwa muda wa miezi mitatu,” alisema Mbugua.

Mkuu huyo wa kaunti aliwapongeza wahudumu wa afya kwa kuitikia wito wa kumaliza mgomo kwa haraka.

“Nashukuru madaktari na wale wafanyikazi wa afya kwa kuwa wakati mgomo wa madaktari ulianza hapa nchini, wao walikubali kukaa chini na kufikia makubaliano na mgomo katika kaunti hii uliisha chini ya siku kumi,” alisema Mbugua.

Baadhi ya wa viongozi wa serikali ya kaunti waliohudhuria shughuli hiyo ni pamoja na Mbunge wa Nakuru Mashariki David Gikaria na Mbunge wa Nakuru Magharibi Samwel Arama.