Hoteli mmoja ya kifahari katika Kaunti ya Mombasa imeripotiwa kukumbwa na mazingira duni, kama vile kuwepo kwa kunguni na makombamwiko katika vyumba vya kulala.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Mteja mmoja aliyelala katika hoteli hiyo ya Mombasa Beach, alilalamikia kuwepo kwa makombamwiko katika vyumba hivyo, pamoja na vyoo vichafu.

Hoteli hiyo ambayo iko chini ya mwavuli wa Kenya Safari Lodge, ambalo ni shirika linalomiliki hoteli mashuhuri hapa nchini, ikiwemo Hoteli ya Ngulia Safari na ile ya Voi Safari, imeonekana kukumbwa na mazingira yasiyoridhisha.

Baadhi ya wafanyakazi katika hoteli hiyo wamekiri kuwa na wakati mgumu sawia na vifaa duni vya kufanyia kazi.

Hata hivyo, mkurugenzi mkuu wa shirika hilo la Kenya Safari Lodge, amesema kuwa ataliangazia swala hilo.

Akizungumza kwenye mahojiano na mwandishi huyu siku ya Jumatano, Timothy Mbogho, aliahidi kuboresha utoaji wa huduma katika hoteli hiyo, pamoja na kuwanunulia wafanyikazi vifaa vipya.

Waziri wa Utalii nchini Najib Balala, alikiri kuwepo na huduma duni katika hoteli hiyo, alipoizuru mapema mwakani.

Balala alisema kuwa hali hiyo imechangiwa na upungufu wa fedha uliosababishwa na kudorora kwa sekta ya utalii nchini.

Aidha, aliwaomba wateja radhi kwa niaba ya hoteli hiyo, na kuongeza kuwa kumekuwepo na mipango ya kuuzwa kwa hoteli za Safari Lodge, lakini kufikia sasa mipango hiyo haijatimia.

Mombasa Beach ni miongoni mwa hoteli za kifahari zinazopatikana katika mandhari mazuri ya ufuo wa Bahari Hindi, katika eneo la Pwani.