Usambazaji wa maji katika gereza kuu la Naivasha umesimamishwa baada ya shirika linalosambaza umeme nchini Kenya Power, kukatiza huduma hizo kwenye bwawa hilo kutokana na deni la Ksh. 900,000.
Hatua hiyo inahatarisha afya ya zaidi ya wafungwa elfu tano pamoja na familia za askari wa kulinda magereza kutokana na ukosefu wa maji safi ya matumizi, huku hatua hiyo pia ikiadhiri hata gereza ndogo la mji huo.
Sasa inahofiwa huenda mkurupuko wa maradhi ukazuka kufuatia shida hiyo huku usimamizi wa gerea hilo ukianza mbinu za kutafuta maji maeneo mengine.
Afisaa mkuu msimamizi wa gereza hilo Patrick Mwenda alisema: “Huduma za stima zilikatizwa Jumanne jioni, tukio ambalo limekwamisha shughuli za kawaida eneo hili.”
Hata hivyo Mwenda alisema kwa sasa wananunua maji ya matumizi ya jikoni kutoka kwa wachuuzi kabla ya hali ya kawaida kurejeshwa.
Kwa upande wake afisa msimamizi wa maswala ya afya wilayani Naivasha Dkt Oren Ombiro amesema maafisa wa afya watafika gerezani humo ktadhmini jinsi ya kuzuia magonjwa kama vile ya kipindu pindu kulipuka, ikizingatiwa visa kadhaa vimeripotiwa kuzuka mjini humo.