Share news tips with us here at Hivisasa

Huenda Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hasan Joho, Gavana wa kaunti ya Kilifi Amason Kingi na mwakilishi wa wanawake wa kaunti ya Kilifi Aisha Mwajuma wakafunguliwa mashtaka ya kuvuruga amani wakati wa uchaguzi mdogo wa Malindi uliofanywa tarehe 7 mwezi huu.

Kulingana na mshirikishi wa kanda ya Pwani Nelson Marwa, viongozi hao aidha walihusika kwa kuleta vijana ambao walionekana wakitumia fujo wakati zoezi hilo lilikuwa likiendelea.

Aidha, Marwa amesema kuwa huenda kundi la vijana la Wakali Kwanza walitumika katika kuvuruga amani katika uchaguzi huo, jambo ambalo ameahidi kulifanyia uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria viongozi hao iwapo itabainika walihusika.

“Ni jambo la aibu sana kuwa kuna baadhi ya viongozi walifadhili vijana ambao walikuwa wakiwavua kina mama nguo na kuwapiga,” alisema Marwa.

Kwa sasa Mshirikishi huyo ametoa wito kwa inspekta generali wa polisi Joseph Boinet kufika Malindi na maafisa wake ili kubaini wenyewe kutoka kwa wakazi jinsi mambo yalivyokuwa.

Picha: Mshirikishi wa kanda ya Pwani Nelson Marwa. Anawataka viongozi wa eneo hilo la Mombasa kuchukuliwa hatua kwa kuzua vurugu wakati wa uchaguzi wa Jumatatu. Maktaba.