Huku serikali za kaunti zikijizatiti kuimarisha hali ya utoaji huduma za afya kote nchini, baadhi ya mipango ya maendeleo inayoanzishwa na serikali za kaunti inazidi kufifia huku mingi ya mipango hiyo kama zahanati zikionekana kuanguka pasi kukarabatiwa kikamilifu.
Kaunti ya Kilifi ni mojawapo ya kaunti ambazo zinajitahidi katika kuhakikisha kuwa hali ya afya inaimarika zaidi kwa kujenga vituo vya afya maeneo ya mashinani chini ya usadizi wa serikali kuu ambayo ilianzisha ujenzi wa zahanati moja katika eneo la Ndigiria eneo la Bamba.
Kituo hicho ambacho kilianzishwa mnamo mwaka wa elfu mbili na mbili chini ya wizara ya afya na ambacho kwa sasa kiko chini ya usimamizi wa idara ya afya katika kaunti ya kilifikwa sasa kinakumbwa na matatizo si haba.
Kulingana na wakazi wa eneo hilo, kituo hicho kwa sasa hakijakamilika licha ya serikali ya kaunti ya kilifi kusema kuwa chini ya serikali ya ugatuzi hali ya afya kote mashinani itaimarika kwa kiwango kikubwa kwa kukarabatiwa na hata kuongezwa kwa idadi ya vituo vya afya ili wakazi wasiwe na wakati mgumu wa kutafuta huduma za afya.
Mama Sidi Mwachiro mwenye umri wa miaka arubaini na sita mzawa wa eneo la Ndigiria kaunti ndogo ya Ganze anasema kuwa iliwabidi waaandamane mnamo mwaka juzi hadi katika hospitali kuu ya kaunti ndogo ya Bamba kama njia mojawapo ya kuwasilisha lalama zao kwa Daktari mkuu wa hospitali hiyo.
Mama huyo pia amesema kuwa hospitali hiyo kwa sasa sehemu za hospitali hiyo zimeanguka jambo ambalo limewalazimu wahudumu wa afya katika hospitali hiyo kutumia vyumba viwili pekee.
Karisa Mwaringa ambaye alikuwa mlinzi wa zahanati hiyo anasema kuwa baadhi ya wanakamati simamizi wa zahanati hiyo walianza kuchua mali ya hospitali hiyo, mali kama vile mawe ya ujenzi, simiti, mbao na vitu vyengine na kupeleka kwenye majumba yao hatua ambayo anasema ilianza kuleta mgawwanyiko miongoni mwao ambayo ilizua chuki.
Mwaringa pia ansema kwamba tangia kuanza kwa mgawanyiko miongoni mwa wanachama wa kamati simamizi, ndio iliakuwa mwanzo wa kusambaratika kwa huduma za hospitali hiyo huku wauguzi wakianza kutekeleza jukumu lao kwa uzembe kiasi cha mama mjamzito kujifungua nje ya zahanati hiyo pasi kushuhulikiwa na muuguzi huku akiwa katika hatari ya kuvamiwa na wanyama wa pori wanaotoroka mara kwa mara kutoka mbuga ya wanyama ya Tsavo Mashariki.
Wakazi hao sasa wameitaka serikali ya kaunti kuangazia miradi ya maendeleo ili kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.