Hazina kuu ya Kitaifa imetakiwa kusitisha usambazaji wa fedha katika kaunti zinazotumia fedha zake vibaya.

Share news tips with us here at Hivisasa

Naibu mwenyekiti wa Chama cha Mahasibu nchini ICPAK, Julius Mwatu amesema kuwa kaunti nyingi humu nchini huvuja mamilioni ya fedha na kushindwa kuboresha huduma msingi kwa wakazi mashinani, na hakuna hatua mwafaka zinazochukuliwa dhidi ya magavana ambao ndio wahusika wakuu.

Akizungumza katika Kongamano la Mahasibu siku ya Alhamis mjini Mombasa, Mwatu amesema kwamba magavana wamejiweka vileleni na kuendelea kutumia fedha za umma kama mali yao ya kibinafsi, hali iliyopelekea wakazi wengi kulalamikia hali duni ya maisha mashinani.

Afisa huyo amemtaka waziri wa hazina kuu ya Kitaifa Henry Rotich kutekeleza jukumu hilo ili kuyanusuru mamilioni ya fedha za umma ambayo yamekuwa yakifujwa na magavana katika kaunti hizo na vile vile kuwachukulia hatua za kisheria Magavana ambao wametumia fedha za umma vibaya.

"Tunamtaka Waziri wa fedha nchini kuzuia usambazaji wa fedha za umma kwa serikali za kaunti zinazotumia fedha vibaya hadi magavana watakapoeleza jinsi fedha hizo zinavyotumika," alisema Mwatu.

Mwatu ameshikilia kwamba bila ya hatua mwafaka kuchukuliwa kuhusu maswala ya usimamizi wa fedha katika kaunti ili kuukabili ufisadi uliyozagaa basi wakenya mashinani watakosa kutambua umuhimu wa ugatuzi.

Wanachama wa ICPAK wakongamana katika hoteli moja mjini Mombasa kujadili maswala muhimu ya utumizi wa fedha za umma na jinsi ya kuchukuliwa hatua viongozi wanaofuja mali za umma.