Hafla ya kukusanya maoni kutoka kwa wakaazi wa Kisii ambayo ilifanyika hii leo, siku ya leo Jumanne katika ukumbi wa Cultural Centre imeshuhudia watu wachache sana ambao walihudhuria kongamano hilo.

Share news tips with us here at Hivisasa

Kampeni hiyo ambayo imekuwa ikiendelea kwa mda sasa kwenye kaunti mbali mbali kote nchini, iliweza kuhudhuriwa naye mwenyekiti wa pesa za maendeleo za maeneo bunge maarufu kama CDF, Elias Mbao pamoja na mbunge wa eneo bunge la Nyaribari Masaba ambaye pia ni mwanachama wa kamati teule ya bunge inashughulikia pesa hizo za CDF ambaye pia anawakilisha kaunti mbili za eneo la Gusii; Kisii na Nyamira.

Ukumbi huo ambao kwa kawaida hujaa pomoni kunapokuwa na hafla kama hizo, ulijazwa nusu, ambapo mwenyekiti Mbao alivilaumu vyombo vilivyowajibishwa kusambaza ujumbe huo kwa kutofanya kazi yao kikamilifu.

Hata hivyo, wengi waliohudhuria kongamano hilo waliunga mkono kuwe na pesa hizo za maendeleo ya maneo bunge, ila wakapendekeza kubadilishwe watu na wasimamizi ambao wanadaiwa kuwa na uhusiano na wabunge wa maeneo ya uwakilishi.

Hafla hiyo ya kukusanya maoni imekuwa ikikusanya maoni kutoka kwa kaunti tatu katika kila kikao, ambapo hafla ya leo iliweza kuwakutanisha wakaazi wa kaunti za Kisii, Nyamira pamoja na kaunti ya Migori.