Vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 ndio wanaongoza katika ulaji wa miraa eneo la Pwani. [Picha/ standardmedia.co.ke]
Shirika moja la kupambana na utumizi wa dawa za kulevya limelalamikia ongezeko la idadi ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 wanaojihusisha na ulaji wa miraa katika eneo la Pwani.Mkurugenzi mkuu wa shirika la Reachout Centre Trust Taib Abdurahman amesema kuwa takwimu hizo ni kinyume na hapo awali ambapo watumizi wengi wa mihadarati walikuwa wa umri wa miaka 18 na zaidi.“Kwa sasa vijana wenye umri wa chini ya miaka 18 ndio wanaongoza katika ulaji wa miraa,” alisema Taib.Akizungumza na wanahabari siku ya Jumapili, Taib alisema takwimu zinaonyesha kuwa ukanda wa Pwani una watumizi wa mihadarati takriban laki moja.“Takwimu bado ziko juu sana. Watu zaidi ya laki moja wanatumia mihadharati katika eneo la Pwani. Hii ni aibu kwa umma,” alisema Taib.Taib alisema kuwa kuna haja ya vijana kuhamasishwa kuhusu athari za mihadarati ili kujiepusha na janga hilo.Vile vile, alisema kuwa jamii imekuwa ikipoteza fedha nyingi ambazo zingetumika kuleta maendeleo kugharamia matibabu ya watumizi wa mihadarati.Taib amezitaja kaunti za Lamu, Mombasa na Kwale pamoja na eneo la Malindi kama maeneo yanayoongoza katika utumizi huo wa mihadarati kanda ya Pwani.