Idadi ya watu waliopatikana kuwa na ugonjwa wa kipindu pindu mjini Naivasha imeongezeka na kufikia sita, baada ya watu wengine wawili kupatikana wakiugua maradhi hayo Jumanne.
Siku moja baada ya visa vinne kuripotiwa mjini Naivasha, wagonjwa wawili; mwanamke na mwanamme, Jumanne walikimbizwa katika hospitali kuu ya wilaya ya mji huo ambapo walilazwa huku uchunguzi uliofanywa ukibainisha kuwa walikuwa na ugonjwa huo.
Katika kisa cha kushangaza, visa vyote sita vinahusisha watu wa kijiji kimoja cha Kihoto, ambacho kinapakana na ziwa Naivasha na kwa sasa kinakabiliwa na uhaba wa maji.
Afisa msimamizi wa maswala afya katika eneo hilo Dkt Samuel Mwaura amesema kuwa wanafanya juhudi kuhakikisha hali hiyo inarekebishwa.
"Tunafanya kila tuwezacho ili kuhakikisha kuwa ugonjwa huo umeweza kudhibitiwa," alisema Mwaura.
Mwaura hata hivyo aliwataka wakazi katika mtaa huo kuzingatia usafi kama njia ya kujikinga kutokana na ugonjwa huo ambao husababishwa na uchafu.
Picha: Kulingana na Dkt Samuel Mwaura, idadi ya wale walioathirika na ugonjwa wa kipindipindu imeongezeka hadi watu sita kutoka eneo la Naivasha.