Watoto wanaoranda randa mitaani. [Picha/ capitalfm.co.ke]
Mkurugenzi mkuu wa maswala ya watoto Kaunti ya Mombasa Philip Nzenge amesema kuwa idadi ya watoto wanaoranda randa mtaani imeongezeka jijini Mombasa, huku wengi wao wakiwa wa chini ya umri wa miaka 18.Nzenge amesema kuwa idadi ya watoto hao imeongezeka hasa katika sehemu ya Posta, Mwembe Tayari na Kongowea.Nzenge alisema kuwa asilimia kubwa ya watoto hao ni vijana ambao wametoroka makwao kutokana na hali ngumu ya maisha.“Wengi wa watoto hao hutoroka nyumbani kutokana na hali ngumu ya maisha inayokabili familia maskini,” alisema Nzenge.Akizungumza na wanahabari jijini Mombasa, Nzenge aliwalaumu wazazi kwa kuwatendekeza watoto wao.“Hawa ni watoto wadogo sana ambao wanapaswa kuwa shuleni ikizingatiwa kuwa elimu ya msingi ni ya bure,” alisema Nzenge.Afisa huyo alisema kuwa idara ya watoto inapania kuanzisha zoezi la kuwatambua watoto wanaorandaranda mtaani na kuwarudisha shuleni.Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa dini kuwajibika na kuanzisha mikakati ya kuwaondoa watoto hao mtaani.Baadhi ya watoto waliohojiwa na mwandishi huyu walisema kuwa wao ni mayatima na hawana mtu wa kutegemea.Hata hivyo, kuna wale waliosema kuwa wanalazimika kuomba omba mitaani kwa vile wazazi wao hawana kazi hivyo hawawezi kujikimu kimaisha.