Idara ya Afya katika Kaunti ya Mombasa imesema kuwa itaanza zoezi la kutembea nyumba hadi nyumba kupuliza dawa ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Malaria.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akiongea kwenye sherehe ya maandimisho ya siku ya Malaria duniani mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Mkurugenzi mkuu wa afya katika Kaunti ya Mombasa Dkt Shem Patta alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kudhibiti kuenea kwa maambukizi ya ugonjwa wa Malaria.

Daktari huyo alisema kuwa idadi kubwa ya watoto wachanga na akina mama wajawazito hupoteza maisha yao kwa kuugua malaria.

Patta amewataka wakaazi kutembelea vituo vya afya kupata maelezo zaidi kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na maambukizi ya malaria huku akiwataka kuweka mazingira yao safi hususan msimu huu wa mvua.

“Tunawaomba wakaazi tafadhali hakikisheni mnatembelea vituo vya afya kupata ushauri zaidi wa kiafya. Zoezi la kunyunyuza dawa litafanyika nyumba hadi nyumba ili kuhakikisha kuwa tunaangamiza malaria kabisa,” alisema Patta.

Hata hivyo, amewataka wananchi kushikamana na wahudumu wa afya kikamilifu katika kufanikisha zoezi hilo la kunyunyiza dawa za kudhibiti mbu lililoanza rasmi mjini Mombasa.