Wizara ya afya nchini imezindua kampeni ya chanjo ya Polio nchini, akihimiza wazazi kuzingatia uhumiwa wa chanjo hiyo kwa watoto wao ili kuwaepusha na magonjwa ya kulemaa.
Mkurugenzi mkuu wa idara ya afya kaunti ya Mombasa daktari Khadija Shikely, alisema kuwa chanjo hiyo ina umuhimu mkubwa wa watoto wa umri wa miaka chini ya mitano huku akisisitiza umuhimu wa wazazi kuzingatia chanjo ya polio kwa watoto wao.
Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumanne, Daktari Shikely alisema kuwa tayari maafisa wa afya na wahudumu wako nyanjani na wanatembea nyumba hadi nyumba kuhakikisha kuwa kila mtoto mwenye umri wa miaka chini ya mitano inapata chanjo hiyo huku akiwakosoa wazazi wanadai kuwa chanjo hiyo inadhuru watoto wao.
Alisema kuwa mahabari ya serikali nchini yalifanya utafiti nasaha na kubaini kuwa chanjo hiyo haina madhara yoyote kwa mtoto na ni kinga kwa mtoto wa umri wa miaka chini ya mitano dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayochipuka kila uchao.
Daktari Shikely aliwataka wazazi kuwa katika mstari wa mbele kuhusu kulinda afya bora ya watoto wao na kuwakinga na maradhi mbalimbali yanayochipuka, akisema kuwa serikali imejitolea kuhakikisha kuwa inalinda afya ya kila Mkenya.
"Ningeomba kuwaambia wazazi kuwa wawemakini na afya ya watoto wao na kuwalinda kila uchao dhidi ya magonjwa mbalimbali yanayochipuka na kuunga mkono juhudi za serikali kuu na kaunti ya Mombasa katika kuwahudumia wananchi kwa mambo ya kiafya," alisema Daktari Shikely.