Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya kutoa uangalizi na ukaguzi wa kontena za mizigo inayoingia bandarini imesema kuwa itaendelea kuweka juhudi kuhakikisha kuwa visa vya uagizaji wa mali haramu na udanganyifu vinapungua.

Akiongea na waandishi habari jijini Mombasa, afisa wa ukaguzi na uidhinishaji wa upakuzi na upakiaji wa mali kwenye bandari ya Mombasa Peter Ng’ang’a alisema kuwa mtindo umezuka miongoni mwa waagizaji wa mali kutoka nchi nyingine, ambapo hubandika jina tofauti kwenye kontena na bidhaa ambazo zimepakiwa ndani ya kontena hali ambayo alisema sharti ikome.

Ng’anga alisema kuwa nyingi ya kontena utapata zina karatasi za bidhaa tofauti na zile ambazo ziliandikishwa wakati wa kuagizia.

Afisaa huyo alitoa mfano wa wiki hii ambapo baadhi ya makasha yamenaswa yakiwa na bidhaa ghusi ambazo zimeharamishwa nchini, na kuonya kuwa huenda baadhi ya wahusika wakachukuliwa hatua kali ya sheria ili kukomesha mtindo huo.

Ng’ang’a alikuwa akiongea siku ya Jumatatu bandarini wakati ambapo alionyesha kunaswa kwa zaidi ya makasha thelathini yaliyokuwa yamepakiwa sukari ambayo alisema kulingana na karatasi rasmi zilionyesha bidhaa tofauti na zile zilikuwa ndani ya makasha.