Maafisa wa upelelezi wamepewa siku 30 kukusanya na kuwasilisha ushahidi wote walionao kuhusiana na kesi ya ugaidi na wizi wa mabavu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kesi hiyo inahusisha mshukiwa wa ugaidi, Luqman Khatib, na vijana wengine watano, walionaswa eneo la Majengo mwaka jana.

Agizo hili linajiri baada ya afisa mkuu wa kituo cha polisi cha Urban, Inspekta Gregory Ogola, kuitaka mahakama kumpa muda wa mwezi mmoja ili kukusanya ushahidi huo.

Hii ni baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa kuwasilisha ombi la kuahirisha kesi hiyo kwa kukosa silaha zilizonaswa na washukiwa hao.

Ombi hilo lilipingwa na wakili wa washtakiwa hao Mkan Moris, aliyesema kuwa kesi hiyo imekuwa ikiharishwa kila mara na kuitaka mahakama kuwaondolewa mashtaka wateja wake.

“Waondolee mashtaka wateja wangu kwa sababu upande wa mashtaka unazidi kulemaza kesi hii,” alisema Moris.

Hakimu mkuu mkazi Irene Ruguru alikubali ombi hilo na kutoa muda wa siku 30 kwa upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi wote.

Adha, Ruguru ameongeza kuwa iwapo afisi ya mwendesha mashtaka utashindwa kufanikisha hayo, basi mahakama itafutilia mbali kesi hiyo.

Kesi hiyo itaskizwa kati ya Oktoba 7 na 10 mwaka huu.