Makundi ya wahalifu yanayoaminika kuwaangaisha wakaazi wa Kisauni, Kaunti ya Mombasa bado ni tishio licha ya idara ya polisi kutangaza vita vikali dhidi ya makundi hayo.
Kundi la Wakali Kwanza pamoja na lile la Wakali Wao yanasemekana kuwa hatari zaidi katika eneo hilo huku yakihusishwa na visa vingi vya watu kuporwa mali na hata pia kushambuliwa kwa silaha hatari.
Idara ya usalama katika ukanda wa Pwani imesema kuwa imezindua mbinu mpya za kukabili makundi hayo ambayo yanazidi kuhangaisha wakaazi.
Akiongea katika kikao na wanahabari afisini mwake siku ya Jumatatu, mshirikishi mkuu wa usalama katika ukanda wa Pwani Nelson Marwa alitaja uzembe wa baadhi ya maafisa wa usalama kama kizingiti katika juhudi hizo.
Marwa alisema kuwa idara ya usalama imejihami na vifaa muhimu vya kusaidia katika zoezi hilo na kusema kuwa hakuna kisingizio cha kushindwa kuangamiza makundi hayo haramu.
“Kuanzia leo na kuendelea, yeyote atakayeleta tumbo kwa barabara atapatana na sheria. Tutaungana mkono katika juhudi za kuleta usalama,” alisema Marwa.
Wakati huo huo, Marwa aliongeza kuwa afisi yake iko na magari ya kutosha yatakayotumika katika operesheni hiyo.
Marwa aliyepandishwa cheo hivi majuzi na kuwa mshirikishi wa usalama Pwani baada ya kuhudumu kama kamishna wa Mombasa kwa muda, aliwaonya makamanda wa polisi wanaozembea kazini akisema kuwa hatua za nidhamu zitachukuliwa.
“Kamanda wa polisi hawezi kuwa anakaa mjini Mombasa wakati watu wanasumbuka. Kama umeshindwa na stesheni uondoke mwingine aingie,” aliongeza Marwa.
Makundi ya Wakali Kwanza na Wakali Wao yamegonga vichwa vya habari siku za hivi karibuni baada ya idara ya usalama kusema kuwa yanaendelea kuwa tishio kubwa katika mtaa wa Kisauni na maeneo yaliyo karibu.
Hata hivyo, polisi hapo awali walidai kuwa kuna mwanasiasa mmoja katika eneo hilo anayewafadhili vijana hao, na kuongeza kuwa wanendelea na uchunguzi kabla ya kumkamata.