Idara ya usalama Pwani inaendeleza uchunguzi wake kuhusu mbinu mpya inayotumiwa na wahalifu na magaidi katika kupanga na kutekeleza visa vya uhalifu katika ukanda huu.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mshirikishi mkuu wa utawala eneo la Pwani Nelson Marwa amesema kuwa idara ya usalama inawahusisha wamiliki wa mahoteli na majumba ya wageni katika ukanda huu ambao mara nyingi huwapokea wageni wasiyowafahamu.

Akizungumza alipozuru ufuo wa bahari ya umma ya Jomo Kenyatta al-maarufu Pirates huko Bamburi mjini Mombasa siku ya Jumamosi, Marwa amesema kuwa sio wageni wote wanaozuru eneo hili wanalenga kujivinjari bali baadhi yao wana njama ya kihalifu au kigaidi na watakabiliwa barabara.

Mshirikishi huyo wa utawala eneo la Pwani amewahimiza wageni wanaozuru ukanda wa Pwani kujivinjari msimu huu wa sherehe za Pasaka kamwe kutohofia lolote kwani usalama umeimarishwa.

“Kama idara ya usalama tunachunguza kwa kina njama mpya inayotumiwa na wahalifu na magaidi katika kutekeleza na kupanga njama za kigaidi na lazima watakabiliwa,” alisema Marwa.

Maafisa wa usalama, Askari wa Kaunti, Maafisa wa Shirika la Msalaba mwekundu sambamba na wapiga mbizi na waokoaji wa kukabiliana na majanga wamekita kambi katika ufuo huo wa Pirates ambao unashuhudia idadi kubwa ya watu msimu huu wa Shamra shamra za Pasaka.