Inspekta mkuu wa polisi Joseph Boinnet katika hafla ya awali. [Picha/ nation.co.ke]
Idara ya usalama Kaunti ya Mombasa imepokea boti sita kutoka kwa serikali ya Korea Kusini.Boti hizo zinatarajiwa kutumika katika kuimarisha doria baharini.Akizungumza siku ya Jumatano wakati wa uzinduzi wa boti hizo katika Bandari ya Mombasa, Inspekta mkuu wa polisi nchini Joseph Boinnet alisema kuwa boti hizo zitatumika katika kuimarisha usalama sawia na kuokoa wananchi wanaopatwa na majanga baharini.“Boti hizi zitatusaidia sana katika kuboresha usalama wa majini katika eneo nzima la Pwani. Aidha, zitatumika katika juhudi za uokozi,” alisema Boinnet.Boinnet vile vile alisema kuwa boti hizo pia zitatumika katika kukabiliana na biashara haramu ya kuleta dawa za kulevya nchini kupitia Bahari ya Hindi.“Huu ndio mwisho wa dawa za kulevya kuingia nchini kupitia baharini. Tutatumia boti hizi katika oparesheni ya kuangamiza mihadharati bandarini na baharini,” alisema Boinnet.Aidha, Boinnet amesema kuwa watatumia boti hizo katika kukabiliana na biashara ya vifaa ghusi katika eneo nzima la Pwani.Kwa upande wake, Balozi wa Korea Kusini humu nchini Kwon Young Dae alisema kuwa teknologia hii itaboresha utendakazi katika idara ya polisi nchini.