Idara ya Elimu katika Kaunti ya Mombasa imetoa hakikisho kuwa itashirikiana kikamilifu na maafisa wa afya katika kaunti hiyo kufanikisha zoezi la chanjo ya ukambi.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Jumatatu, mkurugenzi mkuu wa elimu katika Kaunti ya Mombasa Abdikadir Kike, aliitaja chanjo hiyo kuwa ya manufaa kwa watoto, kwa kusema kuwa itaboresha afya zao.

Kike alisema kuwa watoto wengi huathirika na maradhi hayo, hali inayowafanya kutoenda shuleni na hivyo kurudi nyuma kimasomo.

Alisema kuwa chanjo hiyo itawakinga watoto hao dhidi ya maradhi hayo na kuboresha afya yao.

Aidha, aliwaomba wazazi kuwaruhusu watoto wao kupata chanjo hiyo.

"Tuko tayari kushirikiana na maafisa wa afya kuhakikisha chanjo ya ukambi inatolewa kwa watoto wetu shuleni na wale walio nyumbani ili kuwakinga dhidi ya maradhi hayo,” alisema Kike.

Zoezi la kutoa chanjo ya ukambi pamoja na ile ya pepopunda imeanza rasmi siku ya Jumatatu katika maeneo tofauti kote nchini.