Wakimbizi wa ndani kwa ndani kutoka eneo la Nyanza ambao ni waathiriwa na ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 wamewashinikiza viongozi nchini kuchunga matamshi yao na wakome kuwachochea wakenya.
Wakiongozwa na mwenyekiti wao Nelson Owegi na katibu wao Moureen Opondo, wakimbizi hao wameelezea hofu kuhusu cheche za maneno zinazotolewa na wanasiasa kutoka mrengo wa upinzani sawia na viongozi wa serekali, wanapaswa kuhubiri amani na kuwaleta pamoja wakenya wa tabaka mbali mbali.
''Tuna imani serikali kuu itatukumbuka sisi wakimbizi wa kutoka Nyanza katika juhudi za kuwafidia waathiriwa wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu 2007,'' akasema Owegi.
Waathriwa hao wameelezea matumaini kuwa watapata fidia na kutendewa haki jinsi serekali imewaahidi ndiposa waweze kujiendeleza.
Aidha, wametoa wito kwa wanasiasa kukoma kueneza siasa za uhasama jambo ambalo linasabababisha chuki ,matusi na malumbano jambo ambalo linazidi kuwatia uwonga kila uchao.
"Wakati ambapo viongozi wa serikali na wa upande wa upinzani wanapolumbana na kutoa matamshi ya chuki kuhusu ghasia za baada ya uchaguzi, hatua hiyo ni hatari zaidi kwa usalama wa nchi na kwetu sisi wakimbizi wa ndani kwa ndani tunaumia sana moyoni, wakenya wanahitaji viongozi ambao watatuweka pamoja.'' akaongeza Bi. Moureen Opondo.