Hali ya sintofahamu inaendelea kuwaghubikia mamia ya wakimbizi wa ndani kwa ndani huko Mai Mahiu wasijue ni lini watapewa makazi mapya.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Licha ya kesi dhidi ya naibu wa Rais William Ruto na mwanahabari Joshua Sang kukamilishwa Jumanne, waadhiriwa hao bado hawajui ni lini watapewa makazi mahususi.

Wakizungumza katika kambi ya Jikaze Jumatano, waadhiriwa hao wamesema kuwa licha ya kuahidiwa kuwa watapewa mashamba, ahadi hiyo bado haijaafikiwa.

Wakikaribisha hatua ya kubanduliwa kwa kesi hiyo, wahanga hao wamesema kuwa rais na naibu wake walifaa sasa kuwashughulikia ili waweze kujiendeleza kimaisha.

Mwenyekiti wa kambi hiyo Mohammed Ngugi amesema kuwa kuna wakimbizi ambao hawajapata makazi au hata fedha kama fidia iliyotolewa na serikali.

"Tunafurahia uamuzi wa mahakama ya ICC kwa sababu tunataka amani ishamiri taifa hili lakini serikali lazima ihakikishe pia wakimbizi wa kambi hii wamefidiwa kikamilifu," alisema Ngugi.

Naye Patricia Gitau alihoji kuwa jinsi kesi hizo zilivyobanduliwa, ni sharti hata wao wapewe makazi mazuri ili waweze kuishi kama wakenya wengine.