Tume ya uchaguzi nchini IEBC imekosolewa vikali na wafuasi wa CORD hapa Nakuru, kwa madai ya kuhujumu muungano wa CORD kwa kusema baadhi ya sahihi za Okoa Kenya hazikubaliki.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwanaharakati wa ODM Joseph Nderitu amekosoa IEBC akisema kwamba ilifaa kufanya kazi yake kwa wakati unaofaa, ili CORD ipate nafasi ya kurekebisha sahihi hizo mapema.

“Mimi nilikuwa mmoja wa wale ambao waliendea vitabu vya kukusanya sahihi za Okoa Kenya Nairobi, na nimeshiriki kuzikusanya hapa Nakuru. Vije basi, IEBC kajikokota kutoa uamuzi wake? Hii ni njama ya kuua kufanyika kwa kura ya maoni kupitia Okoa Kenya” Nderitu alisema.

Hata hivyo Nderitu alimchangamoto kiongozi wa upinzani Raila Odinga kusimama na usemi mmoja, wa kushinikiza IEBC iende nyumbani.

“Ni kama kuna vita vimezuka kati ya CORD na IEBC, na ili kuvimaliza, tunahitaji demokrasia kwanza katika chama cha ODM, demokrasia ya kuweka mambo wazi kama yalivyo. Kwa sababu kiongozi wetu (Raila) amesema huu ni msumari wake wa mwisho kupiga, lazima aweke mikakati ya kuunganisha CORD iwe kitu kimoja, la sivyo tutabwagwa na Jubilee,” alisema wakati akizungumza mjini Nakuru na mwandishi huyu.

Kulingana na taarifa iliyotolewa Jumanne na IEBC, ni sahihi  891, 598 zinazokubalika, huku kipengele cha katiba 257(4) kikihitaji kampeni kama hiyo kudhibitishwa na sahihi milioni moja za wapiga kura waliojiandikisha.