Makamishna wa Tume ya Uchaguzi na Mipaka nchini IEBC, wamesema kuwa wamejiandaa vyema katika kufanikisha zoezi la usajili wa wapiga kura katika ukanda wa Pwani.
Kamishna wa Tume hiyo Mohammed Alawi, alisema kuwa maafisa wa tume hiyo wamepokea mafunzo maalum ya kufanikisha zoezi hilo mashinani.
Alisema kuwa hatua hiyoitahakikisha kuwa azma ya tume hiyo ya kusajili Wakenya zaidi ya milioni 18 inaafikiwa.
Akizungmza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Ijumaa, Alawi alisema kuwa wameandaa mikakati mwafaka ya kuhakikisha zoezi hilo linafika hadi mashinani na kusajili wa piga kura zaidi kabla ya zoezi la uchaguzi mkuu kufika.
“Tumeandaa mikakati mwafaka ya kuhakikisha kuwa tunazuru hadi mashinani na kuwasajili Wakenya kama wapiga kura. Kiwango tulichopata katika miaka iliyopita ni kidogo mno ikilinganishwa na idadi ya Wakenya wanaomiliki vitambulisho humu nchini,” alisema Alawi.
Aidha, alisema kuwa licha ya tume hiyo kukumbwa na changamoto za kifedha na masuala ya mitambo ya kisasa ya kusajili wapiga kura, wanamatumaini kuwa zoezi hili litafanyika vyema.
Usajili huo wa wapiga kura kote nchini unatarajiwa kuanza rasmi tarehe 15 mwezi Machi mwaka huu wa 2016.