Tume huru ya uchaguzi na uratibu wa mipaka nchini IEBC, sasa yashinikizwa kuanzisha zoezi la hamasa kwa Wakenya kuhusiana na jinsi uchaguzi mkuu ujao utakavyoendeshwa.
Kulingana na kiongozi wa vijana katika eneo la Kisauni Maxwell Masai, kufuatia jinsi zoezi la usajili wa wapiga kura lilivyoendesha idadi kubwa ya Wakenya hasa kaunti ya Mombasa hawajafahamu umuhimu wa zoezi hilo na huenda wakapata changamoto kubwa zaidi wakati wa uchaguzi mkuu ujao.
Akizungumza katika mtaa wa Mtopanga eneo la Kisauni mjini Mombasa siku ya Jumatatno, katika mkutano wa hamasa kuhusiana na maswala ya uongozi, Masai alisema kuwa kuna haja ya tume hiyo kuzingatia swala hilo na kubuni mikakati itakayosaidia Wakenya kufahamu mengi kuhusu jinsi uchaguzi mkuu utakavyoendeshwa.
Wakati uo huo walisuta magavana hususan wa kaunti za Pwani ambayo kaunti zao ziliorodhesha katika ripoti ya kaunti fisadi iliyotolewa na tume ya EACC kuwa wanazidi kurudisha nyuma taifa hili katika maswala ya kimaendeleo kufuatia ufuja wa fedha za umma.
"Tunawaambia wale viongozi wa kaunti za Pwani zilizotajwa kuwa fisadi wanarudisha nyuma maendeleo ya taifa hili na hatua hiyo itasitishwa na wakaazi wakati wa uchaguzi mkuu kwani hakuna kiongozi atakayesalia tutawaondoa madarakani," alisema Masai.
Kiongozi huyo wa vijana sasa anawahimiza wakaazi kuwa waangalifu na viongozi kama hao na kuwabandua uongozi pindi uchaguzi mkuu utakapowadia huku akiwataka kushiriki kikamilifu katika mikutano ya hamasa.