Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, imehimizwa kutenga nyadhifa mbalimbali za uongozi kwa jamii ya watu wanaoishi na ulemavu kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti.
Akizungumza kwenye kikao na wanahabari mjini Mombasa, mshirikishi mkuu wa muungano unaotetea haki za zeruzeru (Albinism Care Foundation) Kaunti ya Mombasa Josphat Musungu, alisema walemavu wamekuwa wakinyimwa nyadhifa hizo na nafasi zao kupewa watu wasio kuwa walemavu.Musungu aliitaja hatua hiyo kama unyanyasaji miongoni mwa jamii hiyo.Alisema kuwa hali ya kutoshirikisha jamii hiyo kikamilifu kwenye nyadhifa mbalimbali za uongozi ifikapo kipindi cha uchaguzi, imechangia walemavu wengi nchini kupitia changamoto za kimaisha.“Walemavu walinyimwa nafasi ya kuwania nyadhifa mbalimbali za uongozi katika uchaguzi uliopita na watu wengine kupewa nafasi hizo. Hilo ni jambo la kuvunja moyo na ningependa kuhimiza IEBC kulichukulia swala hili kwa uzito,” alisema Musungu.
Maelezo ya picha: Mkurugenzi mkuu wa Tume ya IEBC Ezra Chiloba na mwenyekiti Wafula Chebukati wakiwahutubia wanahabari hapo awali. Tume hiyo imetakiwa kutenga nyadhifa mbalimbali za uongozi kwa walemavu.Picha/ mediamaxnetwork.co.ke