Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka IEBC, imesema iko tayari kusikiliza na kushughulikia malalamiko yote ya wadau wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na Cord.
Wakati huo huo, bodi hiyo ya uchaguzi ililaani mapambano kati ya polisi, viongozi wa Cord na wafuasi wao katika makao makuu ya Tume ya IEBC siku ya Jumatatu, kwa kusema kisa hicho hakikufaa kushuhudiwa.
"Tuko tayari kuwafahamisha kuhusu mikakati tuliyoweka kujitayarisha kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017, na kusikiliza na kushughulikia malalamiko yoyote. Muungano wa Cord ni moja ya wateja wetu. Wanapaswa kuhakikisha kuwa tunawahusisha kwa njia yenye manufaa na umoja,” ilisema ripoti iliyotiwa saini na Meneja wa Mawasiliano na Masuala ya Umma katika tume ya IEBC Andrew Limo.
Tume hiyo ilikubali malalamiko yaliyotolewa na muungano huo wa upinzani, na kusema kuwa imeyashughulikia kwa mujibu wa sheria.
"Cord imepinga uamuzi wa tume hii kuhusu kura ya maoni ya Okoa Kenya pamoja na kuzua wasiwasi kuhusu jinsi uchaguzi mkuu uliopita ulivyosimamiwa.
Haya yote ni maswala tuliyoyashughulikia kwa mujibu wa sheria."
"Muungano huo pia ulitaka kujua iwapo makamishna waliopo mamlakani kwa sasa watawajibika katika uchaguzi mkuu ujao, na kupendekeza wabanduliwe. Muungano huo unaelewa vyema mfumo wa kuteuliwa na kuondolewa kwa makamishna wa IEBC, na makamishna wengine wa tume yoyote ile iliyoundwa kikatiba.”
Maafisa wa polisi walitumia vitoa machozi kutawanywa viongozi wa Cord Raila Odinga, Moses Wetangula, Kalonzo Musyoka na wafuasi wao baada ya kujaribu kutumia nguvu kuingia katika afisa za Tume ya IEBC mjini Nairobi siku ya Jumatatu.
Muungano huo umetishia kususia uchaguzi mkuu wa mwaka 2017 iwapo utasimamiwa na makamishna waliopo mamlakani kwa sasa.