Huenda hoja inayojadiliwa bungeni kuwaruhusu wale walio na kadi za kusubiri vitambulisho vya taifa wasajiliwe kuwa wapiga kura ikachangia visa vya udanganyifu wakati wa uchaguzi mkuu ujao iwapo itaidhinishwa.
Mshirikishi wa tume ya uchaguzi na utaraibu wa mipaka katika eneo bunge la Matuga, Jumaa Musa alisema kuwa hatua hiyo inafaa bunge kulithmani kwa kina kabla ya kufanya maamuzi na kuupitisha mswada huo bungeni.
Akiongea na mwanahabari huyu mjini Mombaa siku ya Ijumaa baada ya kukutana na maafisa wengine wa tume hiyo mjini Mombasa, Musa alikariri kuwa kadi hizo za kusubiri vitambulisho hazina nambari za kitambulisho au hata picha ya anayesajiliwa.
“Hatujakataa mipango ya bunge lakini hali huenda ikampa mtu nafasi ya kupiga kura zaidi ya mara moja na kusababisha udangayifu mkubwa na uharaibifu wa kura wakati wa uchaguzi mkuu ujao kwa hiyo sisi tunataka tu bunge kuthmani swala hilo kwa kina,” alisema Musa.
Hoja hiyo iliyowasilishwa bungeni na mbunge wa eneo bunge la kwanza, Ferdinand Wanyonyi inahimiza Wakenya walio na kadi za kusubiri vitambulisho vya taifa wasajiliwe kuwa wapiga kura.
Afisa huyo aliwahimiza wakazi wa Pwani wajitokeze katika afisi za IEBC katika kila eneo bunge ili wasajiliwe kuwa wapiga kura.