Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Mratibu wa tume huru ya uchaguzi na mipaka (IEBC) katika kanda ya bonde la kati David Towett amekariri kuwa wanatarajia kusajili wapiga kura 267,991 katika kaunti ya Nakuru.

Akizungumza kwenye hafla ya kuhamasisha wanahabari kuhusiana na shughuli ya usajili wa wapiga kura kwenye hoteli moja mjini Nakuru jumatatu, Towett alisema kulingana na takwimu za tume hiyo, watu 1,020,148 katika kaunti ya Nakuru walikuwa wamepata vitambulisho kufikia Desemba 31, 2014.

Alikariri kuwa takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa watu milioni 14.3 walikuwa wamejisajili kama wapiga kura hapa nchini kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2013, 91,033 wakiwa kutoka katika eneo bunge la Nakuru Mashariki huku 71,743 wakiwa kutoka eneo bunge la Nakuru Magharibi.

Hayo yamekaririwa huku tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC ikizindua rasmi zoezi la kuwasajili wapiga kura jijini Nairobi.

Ni zoezi ambalo linatarajiwa kudumu kwa mwezi mmoja huku kukiwa na jumla ya vituo 5, 756 vya kuwandikisha wapiga kura waliofikisha umri wa miaka 18 , walio na vitambulisho vya kitaifa.

Kwa muujibu wa Towett, tume hiyo inatarajia kuwasajili wapiga kura milioni 18 kote nchini kabla ya uchaguzi mkuu ujao wa mwaka wa 2017.