Seneta mteule Beth Mugo ameikosoa Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, kwa kile alichokitaja kama kuzembea katika utendakazi wake hasa katika ukanda wa Pwani.
Bi Mugo alidai kuwa baadhi ya viongozi wa mrengo wa upinzani kutoka Pwani wameonekana wakitatiza zoezi la usajili wa wapiga kura bila hatua zozote za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa, Mugo alisema kuwa kunahaja ya kubadilishwa kwa makarani wa IEBC katika eneo la Pwani kufuatia madai kuwa huenda wanatumiwa vibaya na viongozi wa upinzani, hatua aliyoitaja kama njama ya wizi wa kura ifikapo uchaguzi mkuu.
“Ni jambo la kushangaza kuona baadhi ya makarani wa IEBC wakipewa makaazi na viongozi wa mrengo wa upinzani. Hatua hii inadhihirisha wazi kuwa kuna njama ya udanganyifu wa kura ifikapo uchaguzi mkuu,” alisema Mugo.
Aidha, Mugo ameutaka mrengo wa Cord kukoma kueneza uvumi miongoni mwa wananchi kwamba serikali ya Jubilee ina njama ya kuiba kura, na badala yake kujishugulisha na maswala ya kuelimisha Wakenye kuhusu umuhimu wa kupiga kura.