Tume huru ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC, imesitisha huduma ya kutuma ujumbe mfupi kuthibitisha iwapo mtu amesajiliwa kama mpiga kura.
Haya yanajiri baada ya mitambo ya huduma hiyo kukumbwa na hitilafu.
Kulingana na taarifa kwa vyombo vya habari, iliyotumwa na meneja wa mawasiliano na maswala ya umma katika tume hiyo Andrew Limo, IEBC iliafikia uamuzi huo baada ya kubaini kwamba watu ambao wamekuwa wakituma jumbe hizo punde tu baada ya kusajiliwa wameanza kuingiwa hofu kufuatia hali ya kuchelewa kupata majibu.
Tume hiyo hatahivyo imeweka bayana kwamba wananchi watapata fursa ya kuthibitisha kama wamesajiliwa kupitia kwa zoezi lingine litakalozinduliwa baada ya zoezi la kuwasajili wapiga kura kukamilika.
Wakati huo huo, tume hiyo imewahakikishia Wakenya kwamba hali hiyo itaweza kuthibitiwa na kila mmoja aliyejiandikisha kupata fursa ya kushiriki uchaguzi.
Hatua hii inajiri baadaya kushuhudiwa visa vya watu wakiwemo vinara wawili wa mrengo wa Cord Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kupata wamejisajili kutumia nambari moja ya kitambulisho na watu wengine ambao hawawafahamu.