Share news tips with us here at Hivisasa

Kitengo cha kusimamia mipango na kutoa maelezo ya matumizi ya fedha katika serikali IFMIS kimeanza shughuli ya kuhamasisha umma kuhusu jinsi ya kufuatilia zabuni kupitia mtandao.

Hii inakuja baada ya kugundua kwamba njia ya zamani iliyokuwa ikitumika ilikuwa na changamoto nyingi zinazolemaza zoezi hilo.

Akiongea mjini Mombasa siku ya Ijumaa, afisa mkuu wa maswala ya fedha kaunti ya Mombasa Jonathan Nyongesa alisema wameanza kutumia njia hiyo ili kurahisisha huduma wanazotoa.

“Tumeanza huu mfumo mpya wa kutumia mtandao ili wasambazaji bidhaa wapate fursa ya kuhudumiwa haraka wakati wanapotaka zabuni,” alisema Nyongesa.

IFMIS iliandaa kongamana la siku tatu lilioanza mjini Mombasa Alhamisi ambapo wasambazaji bidhaa mbalimbali kutoka eneo hilo walipata mafunzo.

Mkutano ulilenga sana vijana wanaofanya biashara ili kuelewa jinsi ya kuinua biashara zao kupitia mtandao.

Wakati huo huo Nyongesa alisema kuwa serikali za kaunti zitahakikisha kwamba vijana na akina mama wanapewa nafasi ya kwanza wakati wa kutoa zabuni.

“Tumekubaliana kwamba vijana na akina mama watakuwa wanapewa asilimia 30 ya zabuni zinazotolewa na serikali za kaunti,” aliongeza Nyongesa.

Hata hivyo baadhi ya wale walioudhuria kongamano hilo wameilaumu IFMIS kwa madai kwamba ina upendeleo wakati wa kutoa zabuni hizo na kutaka jambo hilo lifanyiwe marekebisho.