Naandika kuhusu mabinti wazembe vyuoni ambao badala ya kutia bidii kusomea mitihani, wako radhi kugawa tunda ili wapite mtihani.
Haina shaka kuwa wanawake wa kisasa “wako juu” yaani wamepiga hatua sio tu kimawazo na kimasomo, bali pia kiuchumi.
Siku hizi ni rahisi kupata wanawake wakisimamia kampuni kubwa na usishtuke kuona idadi ya wanafunzi wa kike wanaohitimu vyuoni ikizidi kuongezeka.
Baadhi ya kozi zina wanawake zaidi wanaohitimu huku idadi ya mabinti wanaoendesha magari barabarani ikiwa kubwa tofauti na miaka ya nyuma.
Kuna wale wanaohoji kuwa wengi wao wanaendesha magari ya waume na wapenzi wao huku wengine wakiwa wamefadhiliwa na akina kaka kupata utajiri.
Hilo hatupingi kamwe! Lakini ukweli ni kuwa kuna idadi nzuri ya vipusa ambao wamejitahidi kwa udi na uvumba kupata kile walicho nacho.
Hata hivyo tunaposherehekea ufanisi huu wa mabinti, bado kuna wale ambao wanafanya kila jitihada kuhujumu nguvu za wanawake katika jamii kwa kuendelea kudumisha ile kasumba kuwa mwanamke hawezi fanikiwa bila kusaidiwa.
Nazungumzia sampuli ya wanawake wasiojiamini kufaulu katika taaluma kwa nguvu zao bila kuanika maembe juu ya paa.
Mabinti hawa ni wadhaifu na hawaamini kuwa wakiwekwa kwenye mizani moja na akina kaka waliofuzu wataibuka washindi na kupata nafasi sawa ya ajira.
Hawa ni vipusa ambao neno bidii halitambuliki vinywani mwao na badala ya kufanya kila juhudi kujipa riziki hata iwe ndogo, afadhali wachapishe picha zao wakiwa uchi mtandaoni kwa matarajio ya kuwanasa mabwenyenye.
Rasimali zao ni sura na makalio wakisahau kuwa hata sokwe anazo.
Muda wao mwingi umetawaliwa na nywele, mavazi na mapambo. Wengine wao wanadhani njia pekee ya kufaidika ni kumnasa kaka kwa ujauzito.
Huyu ni binti ambaye yuko tayari kulala na dume lolote linaloonyesha ishara za mfuko mzito, bila kinga pasipo kujali kuhusu hali yake ya kiafya, mradi mwishowe atashika mimba atakayoitumia kuchuma pesa kutoka kwa mwanamume huyo pindi mtoto anapozaliwa.
Hawa ni wanawake wanaoendeleza ukahaba eti kwa sababu wanawatafutia wanao “maziwa”.
Je, ni kiungo hiki pekee walichonacho? Hawana miguu na mikono kuchuma nayo?
Jibu langu kwao ni kuwa mama mboga, mama pima na mchuuzi pale barabarani pia ana watoto na anatumia mikono kuhakikisha kuwa wanawe wanakula na kwenda shuleni.