Imani ya wakenya kwa mahakama ya juu inahofiwa kudidimia kwa madai kuwa jaji Philip Tunoi alihusika kwenye tuhuma ya kupokea hongo kutoka kwa gavana wa kaunti ya Nairobi Evans Kidero.
Haya ni maneno ya aliyekuwa mwenyekiti wa chama cha mawakili nchini LSK kanda ya bonde la ufa Bernard Ng'etich katika mahojiano na mwandishi huyu Alhamisi hii mjini Nakuru.
Aidha, alikashifu tendo la hati ya kiapo ya Geoffrey Lang’at iliyomshtaki jaji Tunoi kuchukua muda mrefu kuwasilishwa mbele ya mamlaka husika kwani ilikuwa ya mwaka wa 2014 ilhali ilifikishwa kwa jaji mkuu mnamo mwaka jana mwezi wa Novemba.
Amezidi kusema kwamba iwapo jaji Tunoi atapatikana na hatia baada ya uchunguzi, wakenya hawatakuwa na imani na idara ya mahakama na itabidi majaji wengine kuteuliwa.
Kwa sasa jaji Tunoi anasubiri kufika mbele ya idara ya mahakama JSC kujititea na kuelezea upande wake.