Ukitaja ndizi nchini, umetaja kaunti ya Kisii ambayo imejulikana kwa umaarufu wake kwa ukulima wa ndizi.
Unapopanga kusafiri Kisii majirani hawatakuwacha bila semi za “ukumbuke ndizi please”.
Ni sentensi fupi lakini ina uzito wa aina yake kwa wale wanaojali kuutilia maanani.
Milima ya kijani kibichi, rangi ya utajiri, mimea yenye afya, mvua tele vyote ni ishara tosha kuwa umewasili katika nchi ya ndizi hali maarufu ‘ense yomwando’ kwa Kiswahili ‘nchi ya ahadi’.
Ndizi huwa na umuhimu si haba mwilini. Haswa inapoiva rangi yake hupendeza na kuvutia sana. Leo hii nataka kukuelekeza taratibu ili ujue ni kwa nini ndizi hutambulika sana kama chakula cha kwanza kwa jamii ya Abagusii.
Ndizi ni muhimu sana kiafya, husaidia kupunguza viwango vya sukari mwilini na hata uvimbe mwilini.
Fauka ya hayo pia ndizi hupunguza mawazo na zaidi ni dawa ya kuzuia Saratani ya figo. Kulingana na utafiti uliofanywa na chuo kikuu mjini London wanagenzi hao waulibaini kuwa watoto wanaokula ndizi moja kila siku wana uwezo mdogo sana wa kupata ugojwa wa Pumu au Asthma.
Wakati wa kuendesha mgonjwa hupoteza madini ya ‘Potassium’ mwilini hivyo kumfanya kuwa mnyonge ila swala hilo linapata suluhu mwafaka kwani ndizi ina wingi wa madini ya potasiamu na unapoitumia itasaidia pakubwa katika kutibu au kudhibiti kuendesha.
Ni baadhi tu ya umuhimu wa kula ndizi. Kama hujawahi kutembea Kisii, ni wakati wa kupanga safari. Mmea huu huipatia kaunti ya Kisii taswira ya aina yake.