Wanachama wa Kikundi cha Elimu cha Mombasa wameweka ishara za barabarani zinazoonyesha sehemu ya wanafunzi kuvukia katika barabara kuu ya Bondeni, ili kuthibiti visa vya ajali vinavyowaathiri watoto.
Akizungumza siku ya Jumatatu wakati wa zoezi la kuweka ishara hizo, Katibu wa chama hicho Zenuidin Ali, alisema kuwa hatua hiyo ni njia mojawapo ya kuonyesha watoto kuvuka barabara.
Alisema kuwa watoto katika eneo hilo huwa na changamoto wanapotaka kuvuka barabara, kutokana na magari mengi yanayotumia barabara hiyo kuingia na kutoka mjini.
“Serikali ya kaunti inapaswa kuchukua hatua za haraka ili kuthibiti visa vya wanafunzi kuhusika katika ajali za barabarani katika eneo hili,” alisema Ali.
Abdulsalaam Ali, mkaazi wa eneo hilo, alisema kuwa wanafunzi wengi kutoka shule za karibu hutumia barabara hiyo iliyo na shughuli nyingi.
Mkaazi huyo aliitaka serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kushirikiana na chama hicho kuboresha hali za elimu za wananfunzi Mombasa.