Jina Otile Brown sio geni kwa wanaoenzi muziki wa aina ya Bongo flava.
Ni jina ambalo kufikia sasa lina mwaka mmoja katika ulingo wa burudani na tayari limeendelea kuandikisha rekodi kali katika tasnia ya sanaa.
Otile Brown ni msanii wa pili kupewa jina la wanaochipuka kwa kasi baada ya Dazlah kuzagaa kote nchini alipopiga bonge la kollabo na Susumila kwenye ngoma ya Kidekide.
Otile alisema wakati alihitajika kutulia darasani na kusoma kwa bidii, yeye alianza kuandika mashairi ya mapenzi na kisha kumpelekea mamake.
Alisema mamake alishangaa sana kuona kijana wake na umri mdogo alivyokuwa na uwezo wa kubuni mashairi yaliyojaa utamu wa lugha iliyoonyesha mfuatano wa vina.
Otile alisema alianza kuona mafanikio kwenye ulingo wa sanaa baada ya kutoa ngoma na Khaligraph Jones, ngoma ambayo hadi kufikia sasa inaendelea kufanya vyema.
Baadaye aliachilia ngoma mbili moja kwa jina “Alivyonipenda “akiwa amemshirikisha Rabbit King Kaka huku “Pakate” ikiwa single yake ambayo anakiri kuipenda kuliko nyimbo zote alizofanya tangu alipoamua kufanya muziki kama kazi.
Na kama kawaida, kashfa haziachi kuwafuata wasanii. Otile hivi majuzi amesemekana kumuiga Bahati, msanii anayeimba nyimbo za injili.
Otile hata hivyo alitupilia mbali madai hayo na kusema kuwa Bahati kwake sio chochote.
Kashfa hii ilimfanya Otile kuhojiwa mara kadhaa na baadhi ya vyombo vya habari ila alishikilia msimamo wake kuwa yeye anaimba kiana yake wala hawezi kumuigiza msanii yeyote yule.