Gavana wa Mombasa Hassan Joho akiwa katika Mahakama kuu ya Mombasa hapo awali. [Picha/ nation.co.ke]
Jaji anayesikiza kesi ya Gavana wa Mombasa Hassan Joho kuhusu kugushi vyeti vya shule ameitaka kesi hiyo kusikizwa kwa haraka kabla ya uchaguzi mkuu ujao.
Jaji Erick Ogola alisema kuwa iwapo kesi hiyo itakawia kusikizwa, huenda hatua hiyo ikamuathiri Joho kwenye uchaguzi huo.
“Kucheleweshwa kwa kesi hii kuna uwezekano wa kumuathiri Joho hasa katika uchaguzi wa mwezi Agosti,” alisema Ogola.
Kauli ya Jaji Ogola inajiri baada ya mawakili wa Joho wakiongozwa na Julie Soweto kuomba muda zaidi wa kujitayarisha kwa kesi hiyo.
Jaji huyo aliagiza kesi hiyo kusikizwa kwa haraka ili haki na usawa kupatikana kwa muda ufaao.
“Kesi hii yafaa kusikizwa bila kuahirishwa, ikiwezekana kila siku ili iweze kuamuliwa kwa haraka,” alisema Ogola.
Joho anakabiliwa na madai ya kugushi cheti cha shule ya upili.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 30, 2017.