Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Photo/ the-star.co.ke]
Jaji Mugure Thande amedinda kujiondoa kwenye kesi ya kusikiliza kesi ya kupinga ushindi wa Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Mombasa Aisha Mohammed.Jaji Mugure alisema kuwa hawezi kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa sababu hana upendeleo wowote kwa pande zote mbili.Akitoa uamuzi huo siku ya Jumanne, Mugure alisema kuwa jukumu lake kisheria ni kuhakikisha haki na usawa unapatikana katika pande zote kwenye kesi hiyo.Wiki iliyopita Saad Yusuf Saad, ambaye ni mpiga kura katika Kaunti ya Mombasa, aliwasilisha ombi la kutaka Mugure kujiondoa kwenye kesi hiyo kwa kusema kuwa hana imani naye.Saad kupitia wakili wake Tom Ambwere alisema kuwa hana imani na Jaji Mugure kwa madai kuwa hakuna haki na uwazi katika uendeshaji wa kesi hiyo.Wakili Ambwere alisema mteja wake alipoteza imani na Jaji Mugure baada ya kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Jomvu Badi Twalib.