Jengo la Mahakama ya Mombasa. [Picha/ Kenyans.co.ke]
Mpiga kura mmoja amewasilisha ombi la kutaka jaji anayesikiliza kesi ya kupinga ushindi wa mwakilishi wa wanawake Kaunti ya Mombasa Aisha Mohammed kutosikiliza kesi hiyo.Saad Yusuf Saad amemtaka Jaji Mugure Thande kujiondoa kwenye kesi hiyo.Saad kupitia wakili wake Tom Ambwere amesema hana imani na Jaji Thande, kwa madai kuwa hakuna haki na uwazi katika uendeshaji wa kesi hiyo.Wakili Ambwere amesema mteja wake alipoteza imani na Jaji Thande baada ya kutupilia mbali kesi ya kupinga ushindi wa Mbunge wa Jomvu Badi Twalib."Mteja wangu amesema kuwa hana imani na wewe kabisa na anataka ujiondoe kwenye kesi hii,” alisema Ambwere siku ya Alhamisi.Ombi hilo limepingwa na Paul Butti, wakili wa Aisha Mohammed, aliyesema kuwa hatua hiyo itahujumu utendakazi wa Jaji Thande."Hatua hii sio nzuri kwani inakandamiza uhuru wa mahakama. Usikubali ombi lao,” alisema Butti.Butti aidha aliitaja hatua hiyo kama isiyokuwa na msingi wowote.Kwa upande wake, wakili wa IEBC Augustus Wafula amelitaja ombi hilo kama lisilokuwa na uzito wowote na kumtaka Jaji Thande kulipuzilia mbali.Jaji Thande atatoa uamuzi wa iwapo atajiondoa kwenye kesi hiyo tarehe Oktoba 23, 2017.