Jaji Martin Muya wa Mahakama ya Mombasa amepata uhamisho hadi katika Mahakama ya Bomet kufuatia mageuzi katika Idara ya Mahakama nchini.
Hatua hii inajiri baada ya Jaji Mkuu nchini Dkt Willy Mutunga kufanya mabadiliko katika Idara ya Mahakama ambapo majaji 105 wamepata uahamisho.
Jaji Muya anajulikana Kaunti ya Mombasa hasa katika kuendesha kesi za uhalifu, ugaidi na mauaji.
Wiki iliyopita, Jaji Muya alitoa hukumu ya kifo kwa Mohamed Soud, aliyepatikana na kosa la mauaji ya aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la CIPK Sheikh Mohamed Idris.
Katika uhaamisho huo, jaji maarufu Mumbi Ngugi ameondolewa kutoka kwa Mahakama ya Kikatiba na Haki za Binadamu na kuwekwa kuwa kiongozi wa Mahakama za Kericho.
Jaji Richard Mwongo amesalia kuwa kiongozi wa Mahakama Kuu naye Samuel Mukunya na Jaji Abida Aroni wakihamishwa hadi Busia.
Jaji David Majanja amehamishwa hadi Kisumu kuwa kiongozi wa majaji.
Naye Aggrey Muchelule ameteuliwa kuwa kiongozi wa majaji katika Idara ya familia huku Jaji George Odunga akiwa kiongozi wa majaji katika idara ya kutathmini usawa.
Jaji Isaac Lenaola sasa ni Jaji Kiongozi wa maswala ya katiba na haki za Binadamu katika Idara ya Mahakama Kuu.
Majaji wengine walioathirika ni pamoja na Jaji Boaz Olao ambaye amehamishwa hadi Kerugoya , Jaji Msagha Mbogholi ambaye sasa ni Jaji kiongozi wa majaji katika kesi ndogo ndogo na Jaji Nduma Nderi sasa ni jaji kiongozi wa maswala ya ajira na wafanyikazi katika Mahakama ya Nairobi.