Shirika moja la kutetea haki za binadamu limemtaka Jaji mkuu nchini David Maraga kuchunguza baadhi ya mahakama zilizoko mashinani kwa madai ya kutotimiza haki kwa wananchi.
Haya yanajiri baada ya wananchi wengi, haswa wale wanaoishi mashinani, kulalamikia ukosefu wa haki katika mahakama hizo.
Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Haki Africa Hussein Khalid alidai kuwa baadhi ya mahakama hizo zimekuwa zikishawishiwa na wanasiasa na matajiri katika kuwanyanyasa maskini na walala hoi.
Aidha, alisema kuwa hali hiyo imepelekea wananchi kukosa imani na mahakama hizo haswa katika maswala ya ardhi ambayo yamekuwa donda sugu katika ukanda mzima wa Pwani.
“Ni hali ya kusikitisha kuona kuwa mahakama tunazozitegemea kutatua maswala mbalimbali kwa njia ya haki zikitumiwa kunyanyasa wananchi,” alisema Khalid.
Haya yanajiri siku chache baada ya baadhi ya wanaharakati kukamatwa katika Kaunti ya Taita Taveta kwa madai ya kufanya mkutano kinyume cha sheria, na kutozwa bondi ya laki tatu kila mmoja, jambo ambalo limezua hisia mseto miongoni mwa wenzao.