Mnamo Septemba mwaka wa 2014, mwanamume mmoja huko Kinango, Kwale, aligonga vichwa vya habari kote nchini baada ya kunyanyuka na kumcharaza viboko kiongozi wa Cord Raila Odinga pamoja Gavana wa Kaunti ya Kwale Salim Mvurya.
Mwanamume huyo wa makamo kwa jina Lengo Karisa Mdzomba, alikamatwa punde tu baada ya kitendo hicho lakini baadae akaachiliwa kwa madai kwamba hakuwa na akili timamu.
Hata baada ya jina lake kugonga vicha vya habari huku baadhi ya wanahabari wakimtembelea nyumbani kwake huko Kwale kwa mahojiano, wengi wamekuwa wakijiuliza mwanamume huyo alipotea wapi.
Mwandishi huyu alikutana naye mjini Mombasa siku ya Jumanne na kutaka kujua anavyoendelea baada ya muda huo wote.
“Mimi nipo lakini nilitoka huko Kwale na sasa naishi hapa maeneo ya Mtwapa. Maisha yanaendelea salama nashukuru shughuli kama kawaida,” alieleza huku akitabasamu.
Licha ya kwamba kitendo alichokifanya kilimtia aibu, Mdzomba alisema kuwa alishukuru baada ya kuskia kwamba Raila na Mvurya walimsamehe.
“Mimi nikichukua kiboko niwachape sikuwa na fahamu, ndipo baadae nilipoelezewa kile nilichofanya. Nashkuru kwani viongozi hao walinisamehe,” alisema Mdzomba.
Kisa hicho kilitendeka Raila Odinga alipokuwa amezuru eneo hilo katika kampeni ya Okoa Kenya, huku akiandamana na mwenyeji wake Salim Mvurya.
Katika ukanda wa video uliosambaa katika mitandao ya kijamii nchini, Mdzomba alionekana kubeba bakora ndefu na kumchapa Raila kwenye bega kisha akamgeukia Mvurya kabla kukamatwa na maafisa wa polisi.
Hata hivyo, alimueleza mwandishi huyu kwamba ameamua kubadilisha jina lake la kwanza kwani anaamini kwamba lilimletea nuksi maishani.
“Mimi sio Lengo Mdzomba tena, kuanzia leo naitwa Anderson Karisa na nimeokoka. Mimi ni mkristo na naomba Wakenya wote waishi kwa amani,” aliongeza Mdzomba.