Mwanamme mwenye umri wa makamu anaendelea kuuguza majeraha katika hospitali ya Nairobi Womens tawi la mji wa Nakuru baada ya kupokea kichapo kikali kutoka kwa mukewe katika eneo la Free Area, viungani mwa mji wa Nakuru.
Mwanamme huyo aliyeomba kubanwa jina lake alisema kwamba kulizuka hali ya kutoelewana kati yake na mkewe mnamo Jumamosi usiku 12, Machi 2016, wakati alimpata mkewe na mwanamme mwingine chumbani mwao.
“Nilitoka kazini jioni saa kumi na moja, nikampatia mke wangu pesa za chakula cha jioni, na nikatoka nikaenda kupumzika na marafikize mtaani,” jamaa huyo alisema.
Alisema aliporejea mwendo wa saa tatu usiku alimpata mkewe na mwanamme mwingine katika chumba chao, na alipotaka kujua sababu ya mwanamme huyo kuwa kwake majira hayo, akajibiwa kwa ngumi na mateke na wawili hao.
“Niliokolewa na maafisa wa usalama wakati mke wangu na mwanamme huyo walinivamiwa vibaya na kunileta hapa Nairobi Women’s,” akasema.
Kulingana na nesi katika hospitali ya Nairobi Womens Angela Gwaro, anayemtibu, jamaa huyo hali yake ni shwari kwa sasa.
“Hii ni mara ya pili sasa tunapokea kisanga kama hiki katika hospitali hii chini ya muda wa miezi miwili,” Gwaro alisema.